Daily Archives: March 30, 2015
Tanzania yamuunga mkono Sepp Blatter Kinyang’anyiro cha Uraisi wa FIFA mwaka huu Mei.
Leo Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) akiwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi wamezungumzia uchaguzi wa CAF na FIFA.
Rais Tenga ameishukuru familia ya TFF kwa kumuunga mkono katika kugombea tena nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 7 mwaka huu Cairo. Tenga ni mgombea pekee wa nafasi hiyo kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
Pia Rais wa zamani wa TFF Leodgar Tenga amezungumzia msimamo wa bara la Afrika uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa CAF uliofanyika mwaka jana jijini Sao Paulo, Brazil kuwa wanachama wote wa CAF watamuunga mkono Rais wa sasa wa FIFA anayetetea nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika Mei mwaka huu jijini Zurich, Uswisi.
Vilevile Mkutano Mkuu wa CECAFA uliofanyika Desemba 2014 jijini Nairobi, Kenya ulipitisha azimio la kumuunga mkono Joseph Sepp Blatter katika uchaguzi wa FIFA. Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa tamko rasmi kuwa kwa niaba ya TFF atampigia kura Joseph Sepp Blatter.
Sepp Blatter kwa Ufupi.
Joseph “Sepp” Blatter ni raia wa nchi ya Uswisi mwenye miaka 79 sasa. Blatter amekuwa Raisi wa FIFA toka mwaka 1998. Mwaka huo wa 1998 alimpiku aliyekuwa raisi wa chama cha soka Barani Ulaya (UEFA) Lennart Johansson na kuchukua madaraka kutoka kwa bwana João Havelange. Kwa chaguzi za Uraisi wa FIFA, Blatter amechaguliwa mara nyingine 4 sasa (2002, 2007 na 2011) sasa 2015 itakua mara tano mfululizo.
Blatter amekuwa akiandamwa na kashifa nyingi za rushwa, kufuja mali za FIFA na ikiwemo kashfa kubwa ya kubariki kombe la dunia huko Qatar mwaka 2022 kinyume na utaratibu.
Wapinzani wa Sepp Blatter mwaka huu 2015 ni Luis Figo, Jerome Champagne, Prince Ali bin Al-Hussein na Michael van Praag.
- Issa Hayatou raia wa Kameruni, mwenye umri wa miaka 68 amekuwa Raisi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) toka mwaka 1988.


